Jua ya kwamba mambo yanayomtoa Muislamu katika Uislamu ni mambo kumi :
Moja: Ni kumshirikisha Allaah Aliyetukuka katika ibada, Anasema Allaah:
“Hakika Allaah Hasamehi kushirikishwa na Anasamehe yasiyokuwa hayo kwa Amtakaye” (An-Nisaa: 116)
“Hakika
atakayemshirika Allaah, hakika Allaah Amemuharamishia pepo na mashukio
yake ni motoni na hawana madhalimu mwenye kuwanusuru” (Al-Maaidah: 72)
na miongoni mwa hizo shirki ni kuchinja kwa asiyekuwa Allaah kama anayechinja kwa ajili ya majini au makaburi.
Pili:
Mwenye kufanya baina yake na Allaah viunganishi akawa anaviomba
viunganishi hivyo na kuvitaka uombezi na kuvitegemea, basi hakika mtu
huyo amekufuru kwa makubaliano ya wanavyuoni.
Tatu: Asiyewakufurisha washirikina au akawa ana shaka katika ukafiri wao au akaupitisha (akausahihisha ) ukafiri wao amekufuru.
Nne:
Mwenye kuamini kwamba muongozo wa asiyekuwa Mtume Muhammad (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio muongozo ulio kamili kuliko
muongozo wa Mtume au ya kwamba hukmu ya mwengine ni bora kuliko hukmu
yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama yule
anayefadhilisha hukmu za Matwaghuut kuliko hukmu yake Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi mtu huyo ni kafiri.
Tano: Mwenye kuchukia chochote katika aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata akatekeleza amekufuru.
Sita:
Mwenye kufanyia mzaha (shere) kwa chochote katika dini ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au akafanya utani katika thawabu
au katika adhabu za Allaah amekufuru. Na dalili ni neno Lake Allaah:
“Sema: Je, kwa Allaah na Aayah Zake na Mtume wake ndio mukizifanyia mchezo, musitoe udhuru hakika mumekufuru baada ya kuamini.” (At-Tawbah: 65-66)
Saba: Uchawi; na miongoni mwa huo uchawi ni uchawi wa kutenganisha na kupendanisha basi yeyote mwenye kufanya huo uchawi au akauridhia amekufuru. Anasema Allaah:
“Na hawakuwa wakimfundisha huo uchawi yeyote mpaka wamwambie hakika sisi ni mtihani basi usikufuru.” (Al-Baqarah: 102)
Nane: Kusaidiana na kuwa pamoja na washirikina dhidi ya Waislamu, na dalili ni:
“Na atakaye wapenda makafiri (na kuwafanya ni wasiri wao) katika nyinyi basi hakika yeye ni katika wao. Hakika Allaah Hawaongozi madhalimu.” (Al-Maaidah: 51)
Tisa:
Mwenye kuamini ya kwamba baadhi ya watu wanaweza kutoka katika shari’ah
ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama
vile alivyoweza kutoka Al-Khidhr katika shari’ah ya Muusa basi mtu hiyo
ni kafiri.
Kumi: Kuikataa na kuipa mgongo dini ya Allaah Mtukufu na akawa hajifunzi chochote katika dini. Na dalili ni neno Lake Allaah:
“Na
ni nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyekumbushwa Aayah za Mola wake
kisha akazikataa. Hakika Sisi ni wenye kuchukua kisasi kwa watu wabaya.” (As-Sajdah: 22)
Na
wala hakuna tofauti katika mambo haya yanayomtoa Muislamu katika
Uislamu kwa yule anayefanya utani au anayefanya kwa kweli au anayeogopa
ila anayetenzwa nguvu (kama kushikiwa silaha na akalizimishwa kufanya
mambo hayo). Na yote hayo tuliyoyataja ni katika mambo makubwa
yanayohatarisha na yanayotokea sana, kwa hivyo yapaswa kwa Muislamu
kujihadhari nayo na ayaogope kwa nafsi yake.
Twajilinda kwa Allaah kwa yanayopelekea hasira
Zake na adhabu Zake kali na rahma na amani zimfikie kiumbe bora Mtume
Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jamaa zake na
Maswahaba wake wote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni