Yaliyomo
Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) anawasili Misri
Anarudi kwao
Anawasili Makkah
Anaamrishwa amchinje mwanawe
Mama yake Ismaa’iyl na kisima cha Zamzam
Watu wa kabila la Jurhum
Mwambie abadilishe kizingiti
Wananyanyua nguzo za Msikiti
Kisa cha Watu wa ndovu (As habul fiyl)
Kuujenga upya Al-Ka’abah
Wanaishiwa na pesa za halali
Mara ngapi umebomolewa na kujengwa upya?
Inajengwa tena
Hitimisho
Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) alizaliwa katika mji unaoitwa Aar uliopo kandokando ya mto wa Furaat (Euphrates) Al Kufa - Iraq.
Inajulikana
kuwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) aliuhama mji huo na kuishi
sehemu iliyokuwa ikiitwa Haraan na hatimaye akahamia nchi ya Palestina
na huko ndiko alikofanya makao yake ya kuufikisha ujumbe alopewa na Mola
wake.
Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) anawasili Misri
Nabii
Ibraahiym (‘Alayhis salaam) akifuatana na mkewe alikwenda kutembelea
nchi ya Misri, na huko alipokelewa na mfalme wa Misri aliyewaweka ndani
ya qasri yake, na usiku ulipoingia mfalme huyo alijaribu kumdhuru Bibi
Sarah mke wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam), lakini Mwenyezi Mungu
alimkinga bibi huyo na shari hiyo kwa kuufanya mkono wa mfalme upooze
kila anapojaribu kumsogelea.
Alipoona
dalili za qudra ya Mwenyezi Mungu zikimlinda bibi huyo, mfalme akaacha
vitimbi vyake na kuamua kumpa Bibi Sarah zawadi, na zawadi hiyo ni binti
yake aitwae Hajar, na Sarah akaikubali zawadi hiyo na akamuozesha binti
huyo mumewe Ibraahiym (‘Alayhis salaam).
Anarudi kwao
Ibraahiym
(‘Alayhis salaam) akarudi kwao akiwa amefuatana na wake zake wawili,
Bibi Sarah na Bibi Hajar, na kutokana na mke mpya, Mwenyezi Mungu
alimruzuku mtoto wa kiume waliyempa jina la Ismaa’iyl, jambo
lililomfanya Bibi Sarah awe na wivu mkubwa juu ya mke mwenzake, na baada
ya kuamrishwa na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, Nabii Ibraahiym
akamchukuwa Bibi Hajar pamoja na mwanawe Ismaa’iyl aliyekuwa bado
mchanga wakati huo, na kufunga nao Swafari ndefu kutoka Palestina hadi
nchi ya Hijazi (Saudia hivi sasa).
Anawasili Makkah
Alipowasili
Makkahh penye bonde baina ya Swafa na Marwa mahali kilipo kisima cha
maji ya zamzam hivi sasa, na wakati huo nyumba ya Mwenyezi Mungu
(Al-Ka’abah) ilikuwa ni sehemu iliyonyanyuka tu juu ya ardhi,
ikishambuliwa na upepo mkali pamoja na mikondo ya maji ya mvua iliyokuwa
ikizikwanguwa pembe nne za nyumba hiyo.
Hapakuwa
na mtu anayeishi mahali hapo wala nyumba wala maji isipokuwa mti mmoja
alipowaacha mkewe na mwanawe chini yake, akawawekea birika la maji
pamoja na chombo alichowatilia tende ndani yake, kisha akageuka na
kuianza Swafari ndefu ya kurudi Palestina.
Mama
yake Ismaa’iyl alipomuona mumewe akirudi na kuwaacha mahali hapo
walipopafikia baada ya Swafari ndefu iliyowachukuwa siku nyingi njiani,
mahali pasipo na mji wala kijiji. Hapakuwa na hata dalili ya kuwepo mtu
mahali popote karibu na hapo, akamfuata mumewe na kumuuliza:
“Unatuachia nani mahali hapa pasipo na mtu yeyote?”
Akamuuliza hivyo mara nyingi lakini Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) hakumjibu.
Mwisho Mama yake Ismaa’iyl akamuuliza:
“Mwenyezi Mungu ndiye Aliyekuamrisha?”
Nabii Ibraahiym akamjibu:
“Naam, ndiyo.”
Kwa imani iliyothibiti, kwa utiifu mkubwa na kwa moyo uliosalimu amri, Bibi Hajar akamwambia:
“Kwa hivyo Hatotupoteza”.
Hapo
ndipo Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) alipogeuka na kuianza Swafari
ndefu ya kurudi Sham akimuacha nyuma mkewe na mwanawe wa mwanzo na wa
pekee wakati ule, na baada ya kutembea muda kidogo mahali ambapo mkewe
hakuweza kumuona, Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) akageuka nyuma na
kuomba dua ifuatayo:
رَّبَّنَا
إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ
بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ
أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ
الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ
“Mola
wetu! Hakika mimi nimewaweka (nimewakalisha baadhi ya kizazi changu
(mwanangu Ismaa’iyl na mama yake Hajar) katika bonde (hili la Makkahh)
lisilokuwa na mimea yoyote; katika nyumba yako takatifu (ya Al-Ka’abah
utakayotwambia tuijenge).
Mola
wetu! Wajaalie wasimamishe Sala. Na ujaalie nyoyo za watu zieleke kwao
(wapende kuja kukaa hapa ili pawe mji) na uwaruzuku matunda ili wapate
kushukuru.” Ibraahiym: 37
Anaamrishwa amchinje mwanawe
Nabii
Ibraahiym alikuwa mara kwa mara akija Makkahh kuwazuru mkewe na mwanawe
na hapana anayejuwa uhakika wa idadi ya ziara hizo, isipokuwa
wanahistoria wameelezea juu ya ziara nne maarufu.
Ya
mwanzo ni pale alipooteshwa kumchinja mwanawe wa pekee Ismaa’iyl
(‘Alayhis salaam) na mwanawe akakubali kutii amri hiyo, na alipomlaza
mwanawe kifudifudi ili asiuone uso wake asije akamuonea huruma, na baada
ya Ismaa’iyl (‘Alayhis salaam) kutoa shahada, na Ibraahiym kusalimu
amri kwa Mwenyezi Mungu huku akijitayarisha kumchinja mwanawe, Mwenyezi
Mungu akamfunulia Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) kuwa asimchinje
mwanawe na badala yake akamkomboa kwa kondoo.
Kisa hicho kimeelezwa ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu Aliposema:
فَلَمَّا
أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ. وَنَادَيْنَاهُ أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ.
قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا إِنَّا كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ. إِنَّ
هَذَا لَهُوَ الْبَلَاء الْمُبِينُ. وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ
“Basi wote wawili walipojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu), na akamlaza kifudifudi (amchinje).
Pale
pale tulimwita; “Ewe Ibraahiym; Umekwishasadikisha ndoto. (Usimchinje
mwanao).” Kwa yakini hivi ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
Bila shaka (jambo) hili ni jaribio lililo dhahiri, (mtihani ulio dhahiri).
Basi tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu,” Asw-Swaaffaat: 103-107
Mama yake Ismaa’iyl na kisima cha Zamzam
Bibi
Hajar (Mama yake Ismaa’iyl) akawa anakula zile tende alizowekewa na
mumewe huku akimnyonyesha mwanawe, lakini haukupita muda mrefu maji
yakaanza kupunguwa na hatimaye kumalizika, na mwanawe alipoanza kuona
kiu, Bibi Hajar akaanza kuhangaika huku na kule akimtafutia maji.
Akaliendea
jabali lililokuwa karibu yake - ‘Jabal Swafa’ – na kulipanda, na
alipofika kileleni akaanza kutizama huku na kule akitafuta maji au
mSwafara wa watu watakaokuwa na maji, lakini hakuona kitu.
Akateremka
na kuanza kutembea taratibu penye bonde lililopo baina ya jabali Swafa
na jabali Marwa, na alipofika kati kati ya bonde akaanza kukazana huku
akiliendea jabali Marwa na kulipanda, na alipofika kileleni akaanza
kutizama huku na kule, lakini bila mafanikio yoyote.
Anasema Ibni ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam)) amesema:
“Hiyo ndiyo Saayi mnayotembea baina ya Swafa na Marwa.”
Bibni
Hajar aliendelea kufanya hivyo mara saba, na alipokuwa akiliendea
jabali Marwa akasikia sauti ngeni ikimsemesha. Alinyamaza kimya ili
aisikie vizuri huku akitazama mahali alipo mwanawe, akamuona Malaika
amesimama mahali kilipo kisima cha Zamzam hivi sasa, huku akichimba kwa
ubawa wake mpaka maji yalipofurika, ndipo mamake Ismaa’iyl alipoyaendea na kuanza kuyachota kwa mikono yake huku akimnywesha mwanawe na kunywa yeye mwenyewe.
Alipokuwa akinywa na kumnywesha mwanawe, Malaika akamwambia:
“Usiogope - hutopotea, kwani hapa ndipo ilipo nyumba ya Mwenyezi Mungu itakayojengwa na mtoto huyu na baba yake."
Watu wa kabila la Jurhum
Hazikupita siku nyingi na mama yake Ismaa’iyl akajiwa na mSwafara wa watu wa kabila la Jurhum ambao asili yao ni kutoka Yemen
waliokuwa wasafiri waliopiga kambi sehemu ya chini ya mji wa Makkahh
mbali na hapo, na walikuja baada ya kuwaona ndege wakiruka sehemu
aliyopo mama yake Ismaa’iyl wakasema:
“Bila
shaka ndege hawa wameona maji”, na kwa vile inajulikana kuwa sehemu
zile si kawaida kupatikana maji, wakaamua kutuma watumishi wakachunguze
sehemu walipoonekana ndege, na walipokiona kisima cha maji ya Zamzam
wakarudi kuwajulisha wenzao walioamua kukiendea haraka sana, lakini walipomuona mama yake Ismaa’iyl na mwanawe wakamuomba wakae naye wakamwambia:
“Utaturuhusu tukae pamoja na wewe mahali hapa?”
Mama yake Ismaa’iyl akawaambia:
“Nitakuruhusuni, lakini maji haya ni yangu.”
Wakasema:
“Tumekubali.”
Anasema Ibni ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam)) amesema:
“Jambo hilo lilimfurahisha sana mama yake Ismaa’iyl, kwani alikuwa mwenye kupenda watu.”
Mwambie abadilishe kizingiti
Watu
wa kabila la Jurhum wakateremka na kuazisha maisha mepya mahali hapo,
na Nabii Ismaa’iyl (‘Alayhis salaam) akaishi pamoja nao, akajifundisha
kwao lugha ya kiarabu, akajifundisha kuwinda, na alipokuwa mkubwa
wakamuozesha mmoja katika binti zao.
Baada
ya kuishi muda aloishi, mama yake Ismaa’iyl akafariki dunia na
Ismaa’iyl akaendelea kuishi mahali hapo pamoja na watu wa kabila hilo la Jurhum.
Nabii
Ibraahiym alikuja kumtembelea mwanawe katika ziara yake ya pili lakini
bahati mbaya hajamkuta nyumbani na badala yake alimkuta mkewe, na
alipomuuliza mahali alipo Ismaa’iyl akamwambia:
“Ametoka kwenda kututafutia rizki.”
Nabii Ibraahiym akamuuliza juu ya hali zao na mwanamke akamjibu:
“Sisi ni wanadamu na hali zetu ni za dhiki na shida.”
Akaendela kumshitakia hali zao, na Nabii Ibraahiym alipoondoka kurudi nchi ya Palestina akamwambia:
“Akirudi mumeo msalimie kisha mwambie abadilishe kizingiti cha nyumba.”
Aliporudi Nabii Ismaa’iyl (‘Alayhis salaam) alihisi kuwa jambo fulani limetokea nyumbani kwake, akamuuliza mkewe:
“Alikuja mtu hapa?”
Mkewe akajibu:
“Ndiyo,
alikuja mzee mmoja na wasfu wake ni hivi na hivi, akauliza juu yako na
mimi nikamwambia ulipo, akaniuliza juu ya hali zetu, nikamwambia kuwa
sisi ni wanadamu na kwamba hali zetu ni za dhiki na shida.”
Akamuuliza:
“Alikuusia jambo lolote?”
Akajibu:
“Ndiyo, alinambia ukija nikusalimie kisha nikwambie ubadilishe kizingiti cha nyumba.”
Akamwambia:
“Yule alikuwa baba yangu na ameniamrisha nifarikiane na wewe, kwa hivyo rudi kwa wazee wako.”
Baada
ya kumtaliki mkewe wa mwanzo, Nabii Ismaa’iyl (‘Alayhis salaam) akaoa
mke mwingine, na inasemekana kuwa alikuwa binti wa Mudhaadh bin Amru
aliyekuwa Sheikh wa kabila la Jurhum.
Nabii
Ibraahiym (‘Alayhis salaam) akaja tena kumtembelea mwanawe katika ziara
ya tatu, na Swafari hii hajamkuta pia, na alipomuuliza mkewe
akamwambia:
“Amekwenda
kutuletea mahitaji yetu.” Na Ismaa’iyl alikuwa mwindaji anayesafiri
mara kwa mara sehemu za mbali kwa ajili ya kazi yake hiyo na huchukuwa
muda mrefu Swafarini.
Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam) akamuuliza:
“Vipi hali zenu?”
Akajibu:
“Tumesitirika AlhamduliLlaah tumo katika kheri kubwa.”
Akawa anasema hivyo huku akimshukuru Mwenyezi Mungu.
Nabii Ibraahiym akamuuliza:
“Mnakula chakula gani?”
Akajibu:
“Nyama.”
Akamuuliza:
“Mnakunywa nini?”
Akajibu:
“Maji.”
Akamwambia:
“Mola wangu vibariki nyama na maji.”
Anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam): “Siku hiyo hawakuwa na chochote nyumbani kwao.”
Nabii Ibraahiym akamwambia:
“Akirudi mumeo mpe salamu zangu na umwambie akidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yake.”
Aliporudi Ismaa’iyl akauliza:
“Alikuja mtu leo?”
Akajibu:
“Alikuja
mzee mmoja mwenye umbo zuri, akataka kujuwa habari zako, nikamjulisha,
akaniuliza juu ya hali zetu nikamwambia kuwa tupo katika kheri.”
Akamuuliza:
“Alikuusia jambo lolote?”
Akamwambia:
“Ndiyo, yeye anakupa salamu nyingi na anakwambia ukidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yako.”
Akamwambia:
“Yule alikuwa baba yangu na ananiamrisha nikamatane na wewe.”
Wananyanyua nguzo za Msikiti
Nabii
Ibraahiym akaja tena katika ziara yake ya nne, na Swafari hii Ismaa’iyl
alikuwepo nje ya nyumba yake chini ya mti karibu na kisima cha maji ya
zamzam akichonga mshale wake, na alipomuona baba yake akamnyanyukia kwa
heshima kubwa, akamwamkia kama mtoto anavyoamuamkia baba yake wakakumbatiana kisha Nabii Ibraahiym akasema:
“Mwenyezi Mungu amenipa amri.”
Ismaa’iyl akamwambia;
“Fanya kama ulivyoamrishwa na Mola wako.”
Akamwambia:
“Na wewe unisaidie.”
Akamwambia:
“Nitakusaidia.”
Akamwambia:
“Mwenyezi Mungu Ameniamrisha nijenge nyumba mahali hapa.”
Akamuonesha
ile sehemu ya ardhi iliyoinuka karibu na kisima cha maji ya zamzam,
kisha wote kwa pamoja wakaanza kufanya kazi ya kuzinyanyua nguzo za
nyumba na kuijenga Al-Ka’abah, na Ismaa’iyl akawa anamsogezea baba yake
mawe huku Ibraahiym akijenga, mpaka nyumba ilipokamilika. Walikuwa
wakijenga huku wakiomba dua ifuatayo:
“Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga huu Msikiti.”
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَإِذْ
يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ
رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
“Na
Ibraahiym alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al-Ka’abah) na Ismaa’iyl
(pia) (wakaomba wakasema) “Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali
yetu hii ya kujenga huu Msikiti. Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia na
Mwenye kujua.” Ibraahiym: 127
Na Akasema:
رَبَّنَا
وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ
وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ أَنتَ
العَزِيزُ الحَكِيمُ
“Ee,
Mola Wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao awasomee Aya Zako, na
kuwafundisha Kitabu (chako) na hikima (nyingine) na awafundishe
kujitakasa (na kila mabaya) hakika Wewe ndiye Mwenye, nguvu na ndiye
Mwenye hikima.”Al Baqarah: 129
Na
hii ndiyo tafsiri ya hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wasallam)) alipoulizwa juu ya mwanzo wa amri yake akasema:
“Mimi ni dua ya baba yangu Ibraahiym na bishara ya ndugu yangu ‘Iysa (‘Alayhimus salaam).”
Anasema
Ibni ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa baada ya kukamilisha ujenzi wa
Msikiti wa Al-Ka’abah, Mwenyezi Mungu akamuamrisha Nabii Ibraahiym
awatangazie watu waje kuhiji, na Nabii Ibraahiym akasema:
“Ewe Mola wangu vipi itawafikia sauti yangu.”
Akamwambia:
“Juu
yako ni kutangaza tu, na ni juu Yangu kuifikisha,” ndipo Nabii
Ibraahiym alipopanda juu ya kilele cha mojawapo ya milima ya Makkahh na
kupaza sauti yake akisema:
“Enyi watu mumefaridhishiwa Hija katika nyumba kongwe,” na tangazo hilo likamfikia kila kiumbe baina ya mbingu na ardhi.
“Hamuoni
kuwa watu wanauitikia mwito huo kutoka katika kila pembe ya dunia? Na
katika riwaya nyingine; “Na wa mwanzo kuuitikia mwito huo walikuwa watu
wa Yemen."
Kisa cha Watu wa ndovu (Aswhaabul Fiyl)
Abraha Mhabeshi aliyekuwa gavana wa An-Najaashiy katika nchi ya Yemeni iliyokuwa ikitawaliwa na Ethiopia
wakati huo alikuwa akiona wivu kila anapowaona waarabu wakifunga
Swafari ndefu kwenda kuizuru Al-Ka’abah, na kwa ajili hiyo akaamua
kujenga kanisa kubwa kati ya mji wa Sana-a (mji mkuu wa Yemen) kisha akawataka waarabu waache kwenda Makkahh na badala yake wakahiji penye kanisa lake.
Habari
hizo zilimfikia mmoja katika watu wa kabila la bani Kinanah, aliyeamua
kuingia kanisani nyakati za usiku na kulipaka mavi, jambo
lililomghadhibisha sana Abraha aliyekusanya jeshi kubwa lenye idadi ya
askari wanaozidi elfu sitini pamoja na tembo ishirini na mbili na yeye
mwenyewe akiwa juu ya tembo mkubwa sana, na kuelekea nalo Makkahh kwa
ajili ya kuibomoa Al-Ka’abah.
Alipokaribia
Makkahh, penye bonde la Muhsir baina ya Muzdalifa na Mina, tembo mkubwa
akapiga magoti na kukataa kuendelea na Swafari. Ikawa kila
wanapomuelekeza kusini au kaskazini anainuka na kutembea, lakini
wanapomuelekeza upande wa Makkahh anakataa na hupiga magoti.
Wakawa
katika hali hiyo mpaka pale Mwenyezi Mungu alipowapelekea ndege makundi
kwa makundi, wakawapiga kwa mawe ya udongo unaounguza.
Mwenyezi Mungu Anasema:
أَلَمْ
تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ. أَلَمْ يَجْعَلْ
كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ. وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ.
تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ. فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ
“Je! Huoni jinsi Mola wako Alivyowafanya watu wenye ndovu?
Je! Hakujaalia vitimbi vyao kuharibika.
Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi
Wakawapiga kwa mawe ya udongo wa kuchoma.
Akawafanya kama majani yaliyoliwa (yakatapikwa)?” Suratul Fiyl: 1-5
Ndege
walikuwa wakiwajia kwa wingi makundi kwa makundi, mfano wa vijumba
mshale au zuwarde, kila mmoja akiwa amebeba mawe matatu yenye ukubwa
kiasi cha dengu, moja mdomoni na mawili ameyabana mguuni, na kila
anayepigwa na jiwe mwili wake hukatika vipande vipande na kufa.
Si
wote waliopigwa na mawe hayo, walikuwemo wachache walioachwa wakarudi
mbio kuelekea makwao huku wakiangukiana. Ama Abraha, Mwenyezi Mungu
alimsalitishia maradhi yaliyosababisha makucha yake kukatika na
kupukutika huku akirudi alikotoka, na alifariki alipowasili mji wa Sana-a mwili wake ukiwa mfano wa kuku aliyenyonyoka manyoa.
Makureshi, wao walikimbilia sehemu mbali mbali mbondeni na juu ya vilele vya majabali wakihofia maisha yao, na hawakurudi majumbani mwao mpaka baada ya kumalizika yaliyotokea.
Tukio
hili lilitokea mwezi wa Muharram kabla ya kuzaliwa kwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) kwa siku hamsini au
hamsini na tano takriban muwafaka wa mwisho wa mwezi February au mwanzo
wa mwezi wa March mwaka 571 baada ya Nabii ‘Iysa.
Katika tafsiri ya Suratul Fiyl anasema Ibni Kathiyr;
“Hii ni mojawapo ya neema za Mwenyezi Mungu walizopewa Makureshi baada ya kuwalinda na shari walهokuja
nayo watu wa ndovu waliokuja wakiwa na azma ya kuibomoa Al-Ka’abah na
kuiondoa ili isiwepo tena. Lakini Mwenyezi Mungu aliwaangamiza na
kuwalazimisha waliobaki warudi wakiwa wameshindwa juu ya kuwa walikuwa
watu wanaofuata dini ya Manasara na kwa wakati ule wao walikuwa bora
kuliko Makureshi waliokuwa wakiabudu Masanamu, lakini haya yalikuwa ni
matayarisho ya kuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wasallam), kwa sababu kauli nyingi zinasema kuwa katika mwaka ule
alizaliwa.
Kama
kwamba uhakika wa mambo unasema; ‘Enyi Makureshi hamkupata nusura hii
juu ya Mahabeshi kutokana na ubora wenu, bali kwa ajili ya kuilinda
nyumba kongwe itakayopata heshima kwa kuzaliwa hivi karibuni kwa Mtume
wa Mwenyzi Mungu, Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) mwisho wa
MaNabii."
Habari za tukio hili zilienea kila pembe ya ulimwengu wa wakati ule, na kwa vile Wahabeshi walikuwa na uhusiano mzuri na ًWarumi,
Waajemi waliokuwa wakingoja fursa nzuri kama hii wakaingia na kuiteka
nchi ya Yemen kwa haraka sana, na dola mbili hizi (Uajemi na Roma) ndizo
zilizokuwa dola kubwa za wakati ule, na wakati huo huo tukio hili la
kuangamizwa kwa watu wa ndovu liliujulisha ulimwengu juu ya utukufu wa
nyumba ile ya Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeitukuza
na kuiadhimisha, na kwa ajili hiyo atakapotokea yeyote katika watu wake
akasema kuwa yeye ni Mtume, basi tukio hilo linampa nguvu mtu huyo.
Kwa
hivyo ndani ya tukio hili mna hekima iliyojificha ya Mwenyezi Mungu ya
kuwapa ushindi washirikina dhidi ya watu wa imani kwa njia ya kimiujiza.
Kuujenga upya Al-Ka’abah
Mtume
wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) alikuwa na umri wa
miaka thelathini na tano wakati Makureshi walipoujenga upya Msikiti wa
Al-Ka’abah, kwa sababu miaka mingi ilikwishapita tokea Nabii Ismaa’iyl
alipoujenga na hapakuwa na kilichobaki katika jengo hilo isipokuwa rundu
la udongo lenye urefu wa kiasi cha dhiraa sita, bila ya kipaa, jambo
lililowarahisishia wezi kuingia ndani na kuiba hazina zinazowekwa humo.
Na
kwa vile miaka mingi ilikwishapita tokea kujengwa kwake, kanuni za
maumbile zilikwishafanya kazi yake. Kuta zilikuwa na nyufa, na miaka
mitano kabla ya kupewa utume (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) yalitokea
mafuriko makubwa yaliyosababisha maji kuingia ndani ya Msikiti na
kubomoa sehemu kubwa za Msikiti huo, na kwa ajili ya yote hayo Makureshi
wakaamua kuujenga tena Msikiti huo.
Wakakubaliana kuwa zisiingizwe katika ujenzi wa jengo hilo pesa zozote za haramu. Zisiingizwe pesa za mahari ya mzinzi, wala pesa za riba, wala pesa alizodhulumiwa mtu n.k.
Walikuwa
wakiogopa kuubomoa Msikiti na kuanza kuujenga upya wasije wakadhurika,
mpaka alipotangulia Al Walid bin Mughiyrah na kuianza yeye kazi hiyo, na
wenzake walipoona kuwa hapana kilichomsibu, ndipo nao wakaingia kazini.
Wakawa wanaendelea kuubomoa mpaka walipozifikia nguzo zilizosimamishwa
na Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam), kisha wakaanza kuujenga upya
Msikiti huo, na kila kabila likapewa sehemu yake ya kujenga, na kila
kabila lilikuwa likikusanya mawe yake ya ujenzi, na msimamiaji wa ujenzi
alikuwa Mrumi aitwae Baqum.
Kazi
ilikwenda vizuri mpaka ulipofika wakati wa kulirudisha jiwe jeusi
mahali pake, ndipo mzozo ulipoanza kila kabila likataka kupewa heshima
hiyo ya kulirudisha mahali pake.
Mgogoro
uliendelea muda wa siku nne au tano na mambo yakawa magumu hata watu
wakakaribia kutaka kupigana vita, panga mkononi mpaka pale Abu Umayyah
bin Mughiyra Al Makhzumiy alipotoa rai kuwa; wa mwanzo kuingia Msikitini
kupitia mlangoni ndiye atakayeamua baina yao, na wote wakaridhika na
rai hiyo.
Mwenyezi
Mungu akataka Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam)) awe mtu
huyo, na walipomuona tu akiingia, wote kwa pamoja wakapiga ukelele wa
kuridhika:
"Huyu Muaminifu! Sote tumeridhika naye, huyu Muhammad."
Alipojulishwa
juu ya uamuzi huo, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wasallam) (hii ilikuwa kabla ya kupewa utume) alikubali, na kwa utulivu
akaomba kiletwe kitambaa, akakitandaza na kuliweka jiwe jeusi juu yake,
kisha akawataka viongozi wa makabila yote kila mmoja akamate upande wa
kitambaa, kisha wanyanyuwe kwa pamoja. Wakalinyanyua na walipopafikia
mahali pa kuliweka, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wasallam)) akalinyanyua yeye kwa mikono yake miwili na kulirudisha
mahali pake.
Kwa
njia hii Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam)
aliweza kulitatua tatizo lililokaribia kuleta umwagaji wa damu mkubwa
baina ya Makabila ya Kikureshi, na kila mmoja aliondoka hapo akiwa
ameridhika.
Wanaishiwa na pesa za halali
Makureshi
walishindwa kuukamilisha Msikiti baada ya kuishiwa na pesa za halali,
wakaamua kupunguza kiasi cha dhiraa sita upande wa kaskazini mwa
Al-Ka’abah na hii ni ile sehemu inayojulikana kwa jina la Al Hijr (Hijr
Ismaa’iyl) wakashindwa kuunganisha Msikiti pamoja na Hijri Ismaa’iyl
ambayo asili yake ilikuwa imekamatana na Msikiti. Wakaunyanyua mlango
kiasi cha dhiraa mbili kutoka juu ya ardhi asiweze kuingia isipokuwa
wanayemtaka wao tu, na urefu wa jengo ulipotimia kiasi cha dhiraa kumi
na tano wakaezeka sakafu juu ya nguzo sita, na baada ya kumalizika kazi
hiyo, Al-Ka’abah ikawa na umbo la mraba lenye urefu wa mita kumi na
tano, na upande wa jiwe jeusi pamoja na upande wa pili yake (mkabala
wake) pande zote mbili kila moja ilikuwa na urefu wa mita kumi.
Na
jiwe jeusi liliwekwa juu kiasi cha urefu wa mita unusu kutoka juu ya
ardhi, na upande wa mlango na upande wa mkabala wake ukawa na urefu wa
mita kumi kila upande, na mlango ukanyanyuliwa kiasi cha mita mbili
kutoka juu ya ardhi, na upande wa nje ya Al-Ka’abah ikaachwa ikiwa
imezungukwa na msingi ulionyanyuka kutoka juu ya ardhi kiasi cha robo
mita na upana wa kiasi cha nusu mita.
Na
sehemu hii ilikuwa ikiitwa Ash Shadherwan, sehemu ambayo asili yake
ilikuwa ndani ya jengo la Al-Ka’abah, lakini Makureshi iliwabidi waiache
sehemu hii bila kuijenga, na kwa ajili hiyo Msikiti ukawa na umbo la
mraba badala ya umbo lake la asili lililofanana na herufi D iwapo
utaunganishwa na Hijr kama ulivyojengwa na Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam).
Mara ngapi umebomolewa na kujengwa upya?
Inajulikana kuwa Msikiti wa Al-Ka’abah umejengwa kwa mara ya mwanzo na Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam).
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَإِذْ
يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ
رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
“Na
Ibraahiym alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al-Ka’abah) na Ismaa’iyl
(pia) (wakaomba wakasema) “Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali
yetu hii ya kujenga huu Msikiti). Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia na
Mwenye kujua.” Ibraahiym: 127
Imesimuliwa
na Imam Muslim katika Sahihi yake na pia ndani ya vitabu vyengine mbali
mbali vya elimu ya hadithi na vya Siyrah katika mlango ya 'Kubomolewa
na kujengwa upya Msikiti wa Al-Ka’abah' kama ifuatavyo:
Sehemu
kubwa ya Msikiti iliungua wakati Al Hajjaj alipoushambulia akitumia
'Manjaniq' (mtambo wa kutupa mawe uliokuwa ukitumika katika vitani vya
zamani) akitaka kumuuwa ‘‘Abdullaah bin Az-Zubayr bin ‘Awaam (Radhiya
Llaahu ‘anhu) na hii ilikuwa wakati wa utawala wa Yazid bin Mu’aawiyah.
Mwana wa Az-Zubayr (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliuacha Msikiti kama ulivyo mpaka ulipoingia msimu wa Hija wa mwaka ule na watu wakawa wengi, akawakusanya na kuwahutubia, akasema:
"Enyi
watu! Nataka ushauri wenu juu ya Al-Ka’abah. Niuvunje Msikiti wote
kisha niujenge upya au nitengeneze tu sehemu zilizoungua?"
Ibni ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema:
"Mimi ninayo rai, naona ni bora usiubomoe, bali utengeneze tu na uiache kama
ilivyo nyumba waliosilimu watu juu yake, na mawe waliosilimu watu juu
yake, na alitumwa kwa ajili yake nyumba hiyo Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wasallam)."
Mwana wa Az-Zubayr (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema:
"Mmoja
wenu ikiungua nyumba yake hatoridhika kuiacha ilivyo (bila shaka
atapenda kuijenga upya), vipi basi nyumba ya Mola wenu? Mimi nitaswali
Istikhaarah mara tatu kisha nitaamua."
Na
baada ya kukamilisha tatu akaamua kuubomoa, lakini kila mmoja aliogopa
kupanda na kuianza kazi hiyo asije akadhurika, mpaka alipopanda mtu
mmoja na kunyanyua jiwe, akalitupa chini, na watu walipomuona
hajadhurika wakaingia na wao kazini na kuianza kazi ya kuubomoa Msikiti
mpaka walipozifikia nguzo, kisha mwana wa Az-Zubayr (Radhiya Llaahu
‘anhu) akazinyanyua nguzo na kuujenga upya, na alipomaliza akaishonea
Al-Ka’abah pazia, akaujenga Msikiti kama ulivyokuwa wakati wa Nabii
Ibraahiym (‘Alayhis salaam) kisha akasema:
"Nilimsikia
khale yangu (Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anha) akisema kuwa
amemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam))
akisema:
"Ingelikuwa
watu hawakutoka hivi karibuni tu katika ujahilia na ningelikuwa na pesa
za kutosha kuujenga vizuri Msikiti, ningeongeza dhiraa tano na
kuuganisha na Hijri (Ismaa’iyl) kisha nikajaalia mlango kwa ajili ya
watu kuingia ndani yake na mlango wa kutokea."
Na katika riwaya nyingine:
"Makureshi walipoijenga nyumba walishindwa kuikamilisha kwa sababu waliishiwa na pesa."
Na
katika riwaya nyengine kupitia kwa ‘‘Abdullaah bin Abi Bakr (Radhiya
Llaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wasallam)) alisema:
"Na
ningejenga milango miwili, mmoja mashariki na mmoja magharibi ikawa juu
ya ardhi kisha ningeunganisha Msikiti na Hijri Ismaa’iyl."
Akasema ‘‘Abdullaah bin Zubair (Radhiya Llaahu ‘anhu):
"Mimi leo ninazo pesa na siwaogopei watu."
Akaongeza dhiraa tano na akajenga milango miwili, mmoja kwa ajili ya watu kuingia na mwengine wa kutokea.
Inajengwa tena
Alipouliwa
‘‘Abdullaah bin Az-Zubayr (Radhiya Llaahu ‘anhu), Al Hajjaj
akamuandikia ‘Abdul-Malik bin Marawan aliyekuwa Khalifa wa Waislamu
wakati huo na kumjulisha juu ya mabadiliko aliyofanya mwana wa Az-Zubayr
katika Msikiti, na ‘Abdul Malik akamjibu:
"Urefu alouongeza mwana wa Az-Zubayr uache na sehemu aloongeza katika Hijri ibomowe na milango aloiongeza izibe."
Al Hajjaj akafanya kama alivyoambiwa.
Hitimisho
Riwaya zinazokubalika zilizopokewa na maulamaa zinasema kuwa Msikiti umejengwa mara nne.
Ya kwanza ulipojengwa na Nabii Ibraahiym (‘Alayhis salaam).
Ya
pili wakati wa ujahilia kabla ya Uislamu, na Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam)) alishiriki katika ujenzi huo na wakati
huo alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano na katika riwaya
nyingine alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano.
Ya tatu ulipojengwa na mwana wa Az-Zubayr (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Ya
nne ulipojengwa tena na Al Hajjaj baada ya kupewa amri na ‘Abdul Malik
bin Marwaan ya kubomoa zile sehemu zilizoongezwa na mwana wa Az-Zubayr
(Radhiya Llaahu ‘anhu).
Imepokelewa
pia kuwa Haaruun Ar-Rashiyd alitaka ushauri wa kuujenga upya Msikiti
huo na kuzirudisha zile sehemu zilizojengwa na ‘‘Abdullaah mwana wa
Zubayr (Radhiya Llaahu ‘anhu), lakini Imam Maalik akamnasihi kwa
kumwambia:
"Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ewe Amiri wa Waislamu, tafadhali iache nyumba kama
ilivyo, na usiifanye ikawa mchezo kwa wafalme, kila mmoja akaja kubomoa
na kuujenga upya atakavyo, na mwisho wake haiba ya nyumba itaondoka
ndani ya vifua vya watu."
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni